KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC) imetangaza mikakati yake kabambe ili kuhakikisha Tanzania inapata medali kutoka katika Michezo ya 33 ya Olimpiki itakayofanyika Paris 2024.
Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau alisema hayo leo wakati akimkaribisha mgeni rasmi, ambaye ni Rais wa TOC, Gulam Rashid kufungua Mkutano Mkuu wa kamati hiyo mjini hapa.
Tandau amesema kuwa maandalizi ya kushiriki michezo hiyo inaanza mapema ili kuhakikisha nchi yetu inapata medali ya aina yoyote katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Tanzania kwa mara ya kwanza na mwisho ilipata medali kutoka katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Moscow, Urusi mwaka 1980 kutoka kwa Filbert Bayi na Suleiman Nyambui katika mbio za meta 3000 kuruka gogo na maji na meta 5000.
Tandau amesema kuwa tayari TOC imeandaa mashindano maalumu ya michezo ya riadha, ndondi na judo kwa ajili ya kupata wachezaji watakaofuzu kushiriki michezo hiyo ya Olimpiki.
Mashindano hayo maalumu yafanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na ule wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Desemba 17 hadi 18 na wachezaji watakaofikia viwango wataingia kambini na kupata mafunzo maalumu ndani na nje ya nchi ili kufikia viwango vya kushiriki Michezo ya Olimpiki.
Recent Comments