Leo tarehe 9.3.2026 kamati ya Olimpiki Tanzania imetangaza rasmi muongozo na tarehe ya uchaguzi kwa wale wote watakaowania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa kamati ya Olimpiki Tanzania kwa mwaka 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu wa Rais wa kamati ya Olimpiki Tanzania Henry Tandau amesema, “hapo awali kulikua na zoezi la kurekebisha vifungu kadhaa vya katiba ndipo uchaguzi ufanyike, hivyo kupitia mkutano kiliochofanyika tarehe 31.1.2026 Mkoani Morogoro katiba hiyo imepita kwa kauli moja ya wajumbe wote na msajili ameshaitia ithibati.”
Akitoa muongozo wa uchaguzi wa kamati ya Olimpiki Tanzania, Mwenyekiti wa kamisheni ya uchaguzi TOC wakili Ibrahim Mkwawa ameeleza kwa kusema “kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha sheria na kanuni za TOC uchaguzi wa viongozi utafanyika tarehe 12.4.2026 jijini Dar es salaam.”
Amendelea kwa kufafanua utaratibu wa mchakato wa uchaguzi kama ifuatavyo, kuchukua fomu za uchaguzi ni kuanzia tarehe 14.3.2026 mpaka 27.3.2026 katika ofisi za TOC zilizopo Mwananyamala Komakoma na katika ofisi ya TOC iliyopo maktaba kuu Zanzibar. Tarehe 28.3.2026 ni siku ya kurejesha fomu, tarehe 29.3.2026 mpaka tarehe 30.3.2026 kukagua fomu zilizorudishwa, tarehe 31.3.2026 ni siku ya kutoa orodha ya awali ya wagombea. Tarehe 1-3.4. 2026 kamati ya rufaa itapokea rufaa kama zipo. tarehe 4.4.2026 kamati itatoa maamuzi juu ya wagombea na tarehe 7.4.2026 kamati itatoa orodha ya mwisho ya wagombea. Hivyo kuanzia tarehe 7.4.2026 mpaka tarehe 11.4.2026 wagombea watafanya kampeni zao.
Nafasi zinazowaniwa ni kama zifutazo, Rais wa TOC na Makamu wa rais wa TOC, wajumbe wa kamati ya utendaji Tanzania bara watano na Zanzibar watano.
Amemalizia kwa kusema kua wagombea wote wenye nia na waliokidhi vigezo wanakaribishwa sana kuchukua fomu za uchaguzi.
Recent Comments