WAPANDA baiskeli wa Shinyanga wenye kutumia baiskeli za kawaida leo wametia fora katika Tamasha la 21 la Michezo na Utamaduni la Karatu baada ya kushika nafasi nne za kwanza katika kilometa 60 za mchezo huo.
Wapanda baiskeli hao pamoja na kutumia baiskeli za kawaida ambazo wengi wanafikiria kuwa hazina kasi,waliwashinda wenzao wa Arusha waliokuwa wakitumia baiskeli za kisasa, ambazo maalumu kwa ajili ya mashindano.
Katika mchezo huo, Richard Charles, Mashanga Dura, Paulo Mihambo na Lameck Shiwelu wote wa Shinyanga walishika nafasi nne za kwanza kwa kutumia saa 1:48.09.22, 1:48.13.66, 1:48.16.35 na 1:50.49.10, huku nafasi ya tano ikienda Arusha kwa Mussa Hussein aliyetumia saa .1:50.50.10.
Katika riadha, Emmanuel Giniki wa Talent ya Arusha na Jackline Sakillu wa JWTZ nao waling’ara katika mbio za kilometa 10 na tano kwa wanaume na wanawake wakimaliza wa kwanza.
Giniki alimaliza wa kwanza katika mbio za kilometa 10 kwa wanaume akitumia dakika 30:01.82 akifuatiwa na Inyasi Sulle naye wa Talent aliyetumia dakika 30:30.01 huku Josephat Bitemo wa Polisi akimaliza watatu kwa kutumia dakika 31:11.54.
Sakillu alimaliza wa kwanza katika mbio za kilome tano kwa wanawake kwa dakika 15:20.91 wakati mwanariadha chipukizi kutoka Serengeti, Neema Nyaisawa alimaliza wa pili kwa kutumia dakika 15:41.19 na Agnes Protas wa JWTZ alimaliza watatu kwa dakika 15:52.19.
Mbali na riadha na baiskeli pia tamasha hilo lilihusisha mpira wa wavu, soka, ngoma, sarakasi na kwaya kutoka vikundi mbalimbali vya sanaa kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Karatu.
Recent Comments