WACHEZAJI wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 12 ya Afrika (All African Games) itakayofanyika Rabat, Morocco kuanzia Agosti 19 hadi 31 wametakiwa kutokuwa wanyonge kutokana na idadi yao ndogo na badala yake kupambana na kuleta medali.
Tanzania katika michezo hiyo inapeleka timu za michezo miwili za riadha yenye wachezaji sita, huku judo yenye wachezaji watatu, makocha wawili na meneja wa timu pamoja na viongozi kadhaa.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk Yusuph Singo akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema uchache sio hoja kinachotakiwa kwenda kufanya vizuri na kurudi na medali.
“Msijisikie wanyonge kwa uchache wenu, kwani kuna nchi zinaweza kupeleka wachezaji wengi zikatoka kapa, lakini nyinyi wachache kama mtakwenda kupambana na kurudi na medali za dhahabu mtakuwa katika nafasi nzuri kuliko wale waliopeleka wachezaji wengi, “alisema Singo katika hafla hiyo.
Pia aliwataka wachezaji hao kuwa wazalendo kwa kulishindania taifa lao na kuwa na nidhamu wakati wote wa michezo hiyo hiyo na kutothubutu kujaribu kutoroka.
Nahodha wa timu hiyo, Gabriel Gerald akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema watahakikisha wanapambana vizuri na kurudi na medali kutoka katika michezo hiyo, ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema wenyewe wamechangia tiketi tatu katika timu hiyo ili kuhakikisha Tanzania inapeleka wanariadha hao na meneja, Donath Massawe.

Mbali na Gerald wanariadha wengine katika timu hiyo ni Sarah Ramadhani, Natalia Elisante, Benjamin Kulwa, Khamis Gulam na Regina Mpikachai na kocha Mwinga Mwanjala huku wachezaji wa Judo ni Anogisye Fwele, Hamis Ally na Abdulab Alawi na kocha ni Innocent Mallya.
Timu ya judo imeondoka nchini Agosti 14, 2019 wakati ile ya riadha ilitarajia kuondoka Agosti 20 kwenda Rabat, Morocco kushiriki michezo hiyo.