NYOTA wa riadha Ali Khamis Gulam na Winfrida Makenji wameng’ara katika mbio za meta za 100 na 200 katika Mashindano Maalumu kwa ajili ya kusaka viwango vya kufuzu kwa ajili ya kambi ya Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana.
Mashindano hayo ambayo yalifanyika kwa siku tatu, yaliandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na yalianza Desemba 16 na mbali na riadha, pia yalishirikisha michezo ya judo na ngumu iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ndani wa Benjamin Mkapa.
Katika mchezo wa riadha, Makenji alishinda mbio za meta 100 kwa kutumia sekunde 11:80 kwa wanawake wakati Gulam akitumia sekunde 10:40 kwa wanaume.
Katika mbio ya meta 200, Makenji alitumia sekunde 23:80 wakati na Gulam akimaliza mbio hizo kwa sekunde 21:07.
“Kwangu ni mwanzo mzuri wa maandalizi ya Olimpiki ya 2024 na ni mipango mizuri ya Kamati ya Olimpiki Tanzania kuandaa majaribio haya na ninashukuru nimefanya vizuri katika mbio za meta 100 na 200, “alisema Ally Gulam kwa waandishi wa habari.
Katika kurusha kisahani, Mohammed Ibrahim aliibuka kinara akirusha meta 39 na sentimeta 49.
Katika mbio ya meta 1500, Salma Charles Samwel aliibuka mwamba baada ya kutumia dakika 04:32:09 wakati kwa upande wa wanaume, Epimaki Boniface alitumia dakika 3:46:38 akishinda.
Salma alishinda tena meta 800 akitumia dakika 2:13:69 wakati kwa upande wa wanaume, Seleman Khamis alishinda mbio hiyo kwa kutumia dakika dakika 1:54:20.
Twahir Haji Makame alikuwa kinara wa mbio ya meta 400 akitumia dakika 48:50 wakati Jane Maige akishinda mbio hizo kwa wanawake akitumia dakika 56:62.
Joseph Panga aliibuka shujaa wa meta 5000 akitumia dakika 13:59:60 akiwaacha kwa mbali washindani wenzake, Faraja Lazaro, Marco Monko na Dickson Francis.
Katika kutupa mkuki, Dau Dahala aliibuka kinara akirusha umbali wa meta mita 58:12.
Upande wa masumbwi, Rashid Mrema aliibuka kinara kwenye uzani wa feather baada ya kumchapa Yusuph Abdallah.
Ibrahim Maulid alishinda katika uzito wa light baada ya kumchapa Mohammed Hamadi huku Joseph Philip akimchapa David Charles na kuibuka mtemi katika uzito wa light middle.
Katika lightheavy, bingwa wa medali ya shaba katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka huu, Yusuph Changalawe alimchapa kwa KO Hoza Abdallah katika fainali na kutwaa dhahabu.
Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau alisema baada ya mashindano hayo, wale wote watakaofikia viwango waataanza programu maalumu ya mazoezi kujiandaa kusaka viwango vya kushiriki Michezo ya Olimpiki 2022.
Awali, TOC iliweka viwango vyake vya kufuzu ambavyo viko juu ya vile vilivyotolewa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kwa ajili ya kufuzu kushiriki michezo hiyo ambayo Tanzania ina historia ya kutwaa medali mbili za fedha tangu Uhuru.
“Lengo letu ni kujiweka tayari kwa ajili ya michezo hiyo na kikubwa tunataka kurudi na medali na kumaliza ukame wa miaka mingi tangu mwaka 1980 Tanzania ilipopata medali mbili kutoka kwa Bayi na Nyambui Moscow, “alisema Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau.
Recent Comments