VYAMA na Mashirikisho ya Michezo nchini vimetakiwa kuendesha mashindano yao ya taifa ili kuwa na uhalali wa kuchagua Kamisheni zao za Wachezaji.

Hayo yamesemwa leo na Mgeni Rasmi, Henry Tandau wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kamisheni ya Wachezaji uliofanyika katika hoteli ya Kingsway mjini Morogoro.

Tandau, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa TOC amesema Kamisheni za Wachezaji zina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya mchezo husika, kwani zimekuwa zikiwasilisha changamoto, matatizo na mambo mbalimbali kwa mashirikisho yao kwa ajili ya kupata ufumbuzi na kuleta maendeleo ya mchezo husika.

Alisema kuwa kuna baadhi ya mashirikisho au vyama vya michezo, ambavyo vimeshindwa kabisa kuendesha mashindano ya taifa, hivyo vinashindwa kuchagua kamisheni zao za wachezaji, kwani katika kipindi hicho ndio viongozi wa kamisheni wanatakiwa kuchaguliwa.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema kuwa hana uhakika kama wawakilishi hao wa Kamisheni ya Wachezaji kama wanaingia katika mikutano ya Kamati ya Utendaji au Mikutano Mkuu ya vyama hivyo.

Bayi amesema kuwa hana uhakika kama viongozi hao wa Kamisheni ya Wachezaji kama wanawakilisha wachezaji, kwani baadhi yao wamekuwa wakizungumzia matatizo ya vyama badala ya matatizo ya wacheaji, ambao  wao ndio wawakilishi wa wachezaji.

Rais wa TOC, Gulam Rashid alisema kuwa mashirikisho mengi ya michezo nchini haitaki uwepo kwa kamisheni hiyo kwani wanajua wachezaji watajua na kudai haki zao na mahitaji mengine muhimu.

Baadhi ya wachezaji walisema kuwa wengi wao wameshindwa kushirikishwa katika vikao vya Kamati za Watendaji, hivyo kushindwa kuwasilisha changamoto na matatizo wanayokutana nayo katika mchezo wao.

Wakati huohuo, Kamisheni ya Wachezaji itaongezewa wajumbe kutoka watano hadi kufikia tisa, na mmoja asiwe chini ya miaka 16 na chini kabisa awe anashiriki mashindano ya taifa.